TTCL

Makala

on

IHEFU  ni neno linalotokana na asili ya neno la kabila la wasangu ( LIHEFU ) lenye maana ya majani yanayotanda juu ya maji kwa kujisuka. 
Majani hayo yaliyojisuka kwa ustadi wa aina yake  yanauwezo wa kumwezesha mtu yeyote kutembea juu ya majani hayo  huku chini kukiwa na kina kirefu cha maji  yanayotembea  (ingawa ni hatari kidogo).
Eneo la ihefu lililondani ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha linakadiliwa kuwa na ukubwa wa kilometa za mraba 80 na ni eneo ambalo nyakati za masika hujaa maji kupitia  mto Ruaha mkuu kabla ya maji hayo kwenda katika mabwawa ya mtera.
Unavyofika katika eneo la Ihefu ndani ya hifadhi ya Ruaha utastaajabu kuona mbuga kubwa sana inayovutia kwa muonekano  ambayo si rahisi kuona mwisho wake kwa macho ya kawaida na na ndani kukiwa na miti michache sana ambayo huwa kinvuli kwa baadhi ya wanyama.
Ndani ya eneo hilo  Oevu la Ihefu kuna wanyama wa aina mbalimbali wakiwemo pofu,Swala,ngiri, nguruwe,digidigi  na viboko,lakini sehemu kubwa ya eneo hilo la Ihefu  ndani ya hifadhi hiyo lina tawaliwa na makundi ya ndege aina ya Mbuni wenye maumbo makubwa kwa muonekano  na wanaolandalanda  kwa madaha muda wote katika eneo hilo.
Wastani wa joto katika eneo la Ihefu ni nyuzi joto 34(34C), lakini ni vigumu sana kujisikia joto au jua kali ndani ya eneo la Ihefu kutokana na  hali ya hewa yenye  upepo mwanana unaokufanya  usichoshwe mazingira yake ambayo sehemu kubwa ni mbuga kubwa yenye miti michache sana na nyasi fupi.
Nyakati za Kiangazi  ndani ya bonde hilo sehemu kubwa ya maji hukauka kutokana na hali ya mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo kwa kiasi kikubwa yamesababishwa na shughuli za ufugaji wa mifugo ikiwemo ng’ombe kabla ya eneo hilo halijawa eneo la Hifadhi ya Taifa ya  Ruaha .
Kabla ya serikali  kuchukua uamuzi wa kuiondoa mifugo katika eneo hilo la Ihefu kati ya mwaka 2006 -2008 kutokana na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji katika Mto Ruaha mkuu na eneo hilo Oevu la Ihefu,inakadiliwa kuwa zaidi ya  mifugo  milioni moja  ilikuwa ikizagaa kwajili ya malisho nyakati za Kiangazi.

Ikumbukwe kuwa eneo hilo Oevu la Ihefu(Ihefu Swamp) kabla ya kuwa sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya  Ruaha mwaka 2008,awali sehemu ya eneo hilo  lilikuwa likifahamika kama eneo Oevu la akiba la Utengule(Utengule Swamps Game Controlled Area (USGCA) chini ya serikali ya kikoloni ya Uingereza  tangu mwaka 1953 hadi Uhuru.
Na kati ya mwaka 1985 hadi 1995 serikali ya Tanzania ilianzisha jitihada zaidi za uhifadhi  wa eneo hilo na mwaka 1998 serikali ilitangaza rasmi eneo hilo kuwa pori la akiba la Usangu (Usangu Game Reserve). 
Na mwaka 2008,Rais wa serikali ya awamu ya Nne ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete alitembelea eneo hilo na kutoa karipio kali la kuwataka wafugaji waliobaki waondoke haraka na kwenda mikoa mengine kupisha eneo hilo la Ihefu ambalo ni sehemu ya  Hifadhi ya Taifa ya Ruaha  ambayo ni ya pili kwa ukubwa Barani Afrika. 
Imeandaliwa na Ng’oko Innocent

UJUMBE KWA FACEBOOK