TTCL

Habari

Akamatwa akifukua kaburi la Albino. 

on

                                                        
TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 04.01.2017.
Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Mafanikio yaliyopatikana katika Misako ni kama ifuatavyo:- 
KUKAMATA MTUHUMIWA KWA KOSA LA KUFUKUA KABURI.
Mnamo tarehe 04.01.2017 majira ya saa 01:00 usiku huko katika Kijiji cha Mumba kilichopo Kata ya Ilembo, Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la JONAS JOHN [28] mkazi wa Chapakazi alikamatwa na askari Polisi akiwa na wenzake wawili wakifukua kaburi la marehemu SISTER OSISARA aliyekuwa mlemavu wa ngozi (ALBINO) kwa lengo la kuchukua viungo vyake.
Inadaiwa kuwa marehemu alifariki dunia mwaka 2010 kwa ugonjwa wa homa na kuzikwa katika makaburi ya Kijiji cha Mumba. Mtuhumiwa alikutwa na majembe na makoleo ambayo walikuwa wakiyatumia kufukuria kaburi hilo. Baada ya mahojiano mtuhumwa huyo aliwataja washirika wenzake wawili ambao walikimbia baada ya kuwaona askari. Msako mkali wakuwatafuta watuhumiwa unaendelea.
Mnamo tarehe 03.01.2017 majira ya saa 21:30 usiku huko Mtaa wa Makongolosi, Kata ya Makongolosi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la KELVIN KUBANDA [24] mkazi wa Kahama alikamatwa akiwa na bhangi kete 10 sawa na uzito wa gramu 55.
Mtuhumiwa alikamatwa akiwa katika kijiwe cha kuvutia Bhangi. Upelelezi unaendelea.

WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa jamii kuacha tamaa mali/fedha kupitia njia zisizo halali kwani Jeshi la Polisi halitaruhusu wala kufumbia macho vitendo kama hivyo na badala yake wajishughulishe na kazi halali kwa lengo la kujipatia kipato halali kuendesha maisha yao. Aidha Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa vijana na jamii kwa ujumla kuachana na matumizi ya dawa za kulevya kwani ni kinyume cha sheria na ni hatari kwa afya ya mtumiaji. Pia anaendelea kutoa wito kwa wakazi wa Mbeya kutoa taarifa za mtu/watu au kikundi cha watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kwa hatua zaidi za kisheria.

    

    Imesainiwa na:

[DHAHIRI A. KIDAVASHARI – DCP]

KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

UJUMBE KWA FACEBOOK