TTCL

Habari

CHADEMA MBEYA MJINI WAITISHA MAANDAMANO KULAANI SHAMBULIO LA TUNDU LISSU

on

Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Mbeya mjiniObadia Mwaipalu akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani). Baadhi ya Viongozi wa Chadema Wilaya ya Mbeya mjini wakimuunga mkono Mwenyekiti wao alipokuwa akitoa tamko la kulaani shambulio la Tundu Lisuu kwa waandishi wa Habari.

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Mbeya mjini kinatarajia kufanya maandamano ya amani jijini Mbeya ili kupinga na kulaani vitendo viovu vinavyofanyika vikiwemo shambulio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antipius Lissu na watu wasiojulikana.

Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya mjini, Obadia Mwaipalu alisema Chama kimekusudia kuandika Barua kwa Jeshi la Polisi la kuomba kibali cha maandamano yatakayofanyika Ijumaa Septemba 15, Mwaka huu.

Alisema baada ya maandamano hayo yataanzia katika Ofisi za Chadema zilizopo Makunguru na yataishia katika Viwanja vya Shule ya Msingi RuandaNzovwe ambapo pia Ibada maalum itafanyika ikihusisha dini zote lengo likiwa ni kumuombea afya njema Tundu Lissu.

Aliongeza kuwa maandamano hayo yatakuwa ya amani hivyo hatarajii Jeshi la Polisi kupinga au kuzuia bali linapaswa kutoa ushirikiano na kuyalinda ili walio kwenye maandamano wasiweze kupata madhara na kwamba lengo lao ni kulisaidia Jeshi hilo na Serikali kukemea vitendo hivyo.

Mwaipalu alisema mbali na kulaani tukio la kupigwa Risasi kwa Tundu Lissu pia Maandamano hayo yatatumika kupinga matukio ya Utekaji wa watu, mauaji yanayoendelea, kupotea kwa viongozi na uhalifu mbali mbali unaoendelea nchini.

Mwenyekiti huyo pia alisema Chama kinalaani kwa nguvu zote tukio lilitokea na kulitaka Jeshi la Polisi kutumia nguvu kama iliyotumika kuhakikisha mauaji ya Kibiti yanaisha kuwasaka waliohusika na kumpiga Risasi Tundu Lissu.

Aliongeza kuwa Serikali inapaswa kuwahakikishia Ulinzi na usalama wa Wapinzani kuanzia Viongozi wa Serikali za Vijiji, Mitaa, Madiwani na Wabunge ili waishi maisha yasiyo na mashaka kama ilivyosasa.

Mwisho.

UJUMBE KWA FACEBOOK