TTCL

Habari

CWT,WADAU ELIMU KUSHIRIKIANA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WALIMU

on

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Julius Chalya akifungua mkutano wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Rungwe uliofanyika hivi karibuni

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wilaya ya Rungwe Elizabeth Sekile akiongea jambo wakati wa Mkutano wa CWT Wilaya ya Rungwe

Katibu wa CWT Wilaya ya Rungwe Mustafa Mitego akisisitiza jambo kwa Walimu katika Mkutano wa Chama cha Walimu uliofanyika hivi karibuni

Wanachama wa CWT Wilaya ya Rungwe wakiwa wameshikana mikono wakiimba wimbo wa mshikamano kabla ya kuanza kwa mkutano wao

Wanachama wa CWT Wilaya ya Rungwe wakiwa kwenye  mkutano wao

ILI kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili Walimu nchini, Imeshauriwa Chama cha Walimu (CWT), Tume ya Utumishi wa Walimu, Ofisi ya udhibiti ubora na Maafisa Elimu kuwa na vikao vya pamoja wakati wa majadiliano.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Julius Chalya alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa Robo ya kwanza ya Mwaka wa Chama cha Walimu Wilaya ya Rungwe uliofanyika Makandana Tukuyu mjini.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema malalamiko ya Walimu karibu ni yaleyale kila Mwaka nchi nzima wanazungumzia madai na mapunjo mbalimbali hivyo ili kumaliza kabisa migogoro hiyo ni vema Ofisi za Elimu kuwa na vikao vya pamoja na wadau wakiwemo uongozi wa Chama cha Walimu.

Alisema yapo madai mengine ya Walimu yanatokana na kutoelewa vizuri mfumo wa Serikali hivyo hujikuta wakidai kitu ambacho hakipo kwenye mfumo wa ajira jambo linalopelekea kuwepo kwa mlundikano wa malalamiko kitu ambacho vyombo vinavyohusika vingefuatilia madai hayo yasingekuwepo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Rungwe, Mwalimu Elizabeth Sekile akimkaribisha mgeni rasmi alisema changamoto za Walimu zinatokana na Wakurugenzi wa Halmashauri za Rungwe na Busokelo tangu kuteuliwa kwao hawajawahi kuitisha mkutano wa baraza la wafanyakazi ambao ungesaidia kutatua baadhi ya madai.

Alisema pia kumekuwepo na changamoto za ubaguzi wa Walimu kuwapandisha madaraja walimu wapya na kuwaacha wakongwe jambo linalochangia kuwepo kwa manung’uniko miongoni mwa watumishi na kupelekea kupunguza ari ya ufundishaji.

Awali akisoma Risala ya Walimu kwa mgeni rasmi, Katibu wa CWT Wilaya ya Rungwe, Mustafa Mitego alisema Walimu wa Halmashauri za Rungwe na Busokelo wanaidai Serikali zaidi ya Shilingi Milioni 800 ikiwa ni malimbikizo ya kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka huu.

Alisema katika fedha hizo Halmashauri ya Rungwe ni Walimu 1040 ambao wanaidai Serikali shilingi 721,943,853 huku Halmashauri ya Busokelo ikiwa na Walimu 277 wanaodai malimbikizo ya shilingi 104,492,600.

Aliongeza kuwa madai mengine ni pamoja na Walimu waliosimamia mitihani ya Taifa ya darasa la nne mwaka 2015/2016 kutolipwa stahiki zao, Wafanyakazi hodari wa Mwaka 2016/2017 kutolipwa zawadi zao pamoja na Walimu wa Sayansi walioajiriwa kati ya Mwaka 2006 hadi 2016 kutolipwa fedha za kujikimu.

UJUMBE KWA FACEBOOK