TTCL

Habari

HALI SI SHWARI KATI YA HALMASHAURI YA JIJI LA MBEYA NA WAHANGA SOKO LA UHINDINI

on

Sehemu ya Soko la Uhindini likiwa limetelekezwa Eneo la Soko la Uhindini baada ya kufanyiwa usafi Moja ya Vibanda vilivyokuwa vimeanza kujengwa kabla ya kusimamishwa Muonekano wa Vibanda vya mfano kabla ya mchakato kusimamishwa na kumpisha Mwekezaji.

 

MVUTANO mkubwa umeibuka baina ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Wafanyabiashara walioathirika kwa kuunguliwa na Soko la Uhindini miaka saba iliyopita baada ya Wahanga hao kutaka kurudi huku Halmashauri ikidai imempata mwekezaji atakayejenga eneo hilo.

 

Mvutano huo pia unachangizwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla pamoja na Diwani wa Kata ya Sisimba (CHADEMA) Jofrey Kajigili ambaye ameungana na Wafanyabiashara kutaka kurejea katika eneo hilo huku akipingana na maamuzi ya Baraza la Madiwani ya kumpa Mwekezaji.

 

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, Baadhi ya Wafanyabiashara hao walisema hawapingani na maamuzi ya Jiji ya kumuweka mwekezaji kujenga soko hilo ila wanataka waruhusiwe kujenga vibanda vya muda kabla ya Mwekezaji hajaanza.

 

“Hatupingani na Jiji, kwanza ikumbukwe kuwa Tenda ya kumpata Mwekezaji lazima itangazwe pia tushirikishwe sasa wao wamefanya kimya kimya na kutuzuia kujenga kwa madai ya Mwekezaji basi waturuhusu tujenge vibanda vya muda ili akija tumpishe” alisema Mwandambo.

 

Alisema eneo ambalo wanafanyia biashara kwa sasa halina mzunguko mzuri pia usalama wa mali sio mzuri hali inayopelekea kuibiwa kila mara hivyo njia pekee ya kuepuka ni kurudi kwenye eneo lao la awali.

 

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Sisimba, Jofrey Kajigili alisema ni vema Wafanyabiashara wakarejea kwenye eneo hilo wakati Jiji likiendelea na taratibu za Mwekezaji kwani hadi sasa hakuna mkataba uliosainiwa baina ya Halmashauri na Mwekezaji wanaodai amekubali ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa(NHC).

 

Alisema kilichofanyika ni NHC kufika na kuangalia eneo na kuchukua sampuli za udongo na kitendo hicho hakiashirii Shirika kukubali kujenga soko na kwamba hata kama watakubali hawatarajii kuanza mapema hivyo ni vema wafanyabiashara wakaendelea na biashara zao.

 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya alipoulizwa na Wafanyabiashara kuhusu hatima yao katika kikao chake cha kusikiliza kero ambapo Wafanyabiashara hao walimuomba kibali cha kuanza kupanga biashara zao eneo hilo alisema wasubiri kwanza wakae na Uongozi wa Jiji ukiongozwa na Kamati ya Fedha ya Baraza la Madiwani ili kufikia muafaka kabla ya kuanza biashara.

 

“Niwaombe Kamati ya Fedha ikakae na wafanyabiashara hao palepale sokoni ili mkubaliane kwa pamoja kwani mimi sina taarifa na sijapewa wala kuona ramani iliyotolewa na mwekezaji badala yake nilimuona Meya kwenye tv akiwaonesha wawekezaji eneo la Soko” alisema Makalla.

 

Hata hivyo katika kikao cha Kamati ya Fedha na Wafanyabiashara kilichofanyika hivi karibuni sokoni hapo kilishindwa kufikia muafaka baada ya Naibu Meya kuwaambia wafanyabiashara kupisha eneo hilo kwa kuwa Jiji tayari limempa Mwekezaji ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

 

Alisema Shirika la Nyumba limekubali kujenga “Shopping Mall” kwani hivi sasa Jiji halina sehemu nyingine kwa ajili ya kujenga Jengo lenye kivutio kuendana na hadhi ya Jiji hivyo ni vema Wafanyabiashara wakawa wavumilivu.

 

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Vicent Msolwa aliwasihi Wafanyabiashara kupisha eneo hilo ili kuendana na matakwa ya Madiwani na kwamba baada ya Mwekezaji kukamilisha Mradi wahanga watapewa kipaumbele cha kwanza kwa kuzingatia masharti.

 

Aidha kutokana na majibu hayo Wafanyabiashara hao walionekana kutoridhika na hivyo kuamua kumuandikia Barua Waziri Ofiri ya Rais, Tamisemi ili kumuomba kibali cha kufanya biashara kwenye eneo hilo tofauti na mtazamo ya Halmashauri.

 

Walisema Halmashauri imekuwa ikianzisha miradi bila kushirikisha wadau ambao ni wafanyabiashara jambo linalopelekea miradi hiyo kudolola likiwemo Soko la Kimataifa la Mwanjelwa ambalo tangu kukamilika hakuna Biashara inayofanyika.

 

 

 

UJUMBE KWA FACEBOOK