TTCL

Makala

JE UNAYAJUA MAKUMBUSHO YA BABA WA TAIFA MWL. NYERERE MWITONGO –BUTIAMA?(MWALIMU NYERERE MUSEUM  CENTRE).

on

SIKU moja naamua kuweka mikakati akilini mwangu  ni lazima nifike alikozaliwa Baba wa Taifa,Hayati Julius Kambarage Nyerere,huko Butiama Mkoa wa Mara na baada ya miezi mitatu nikaianza safari.
Kabla ya kuanza safari yangu nakutana na wazee mbalimbali  waliowahi kumuona mwalimu na wananisimulia mambo mengi sana,lakini kubwa zaidi linalonigusa akilini mwangu ni kuwa mwalimu Nyerere  aliishi maisha ya kawaida sana.
Nakumbuka oktoba,14 mwaka 1999   wakati mwalimu Nyerere anafariki nilikuwa ndiyo naanza elimu yangu ya  masomo yangu ya sekondari,ilikuwa mchana mara tukasikia kengere inagongwa na wanafunzi wote tukakusanyika mstarini,mara nikamuona mkuu wa shule mwenye asili ya kihindi akitutangazia kuwa kuna msiba mkubwa na imeshatangazwa na Rais kuwa Mwl amefariki huko uingereza.
Ghafla nikanza kupata hofu kubwa  na nilipowaangalia wanafunzi na walimu wote walikuwa na hofu,lakini nakumbuka swali langu la kwanza je tutaishije? Niliamua kuondoka taratibu na kuelekea bwenini hakika nilikosa raha kabisa huku nikiwa na mawazo rukuki ya kitoto je taifa bila mwalimu Nyerere litakuwaje?
Muda mwingi nikawa nakumbuka nyimbo nzuri za kizalendo tulizokuwa tukiimba wakati tukiwa shule ya msingi za kumsifu mwalimu kutokana na jitihada zake  mbalimbali ndani ya Tanzania zikiwemo za kutuletea uhuru ambazo tulikuwa tukifundishwa na walimu mahiri.
Wakati wanafunzi tumepewa siku kadhaa kwajili ya maombolezo ya Kifo cha Mwalimu,mimi na rafiki zangu tukawa tunafuatilia tukio hilo kupitia televisheni,hofu iliniingia zaidi kutokaa na kuona watu wengi wakilia kwa uchungu na maeneo yote ya mitaani karibu na shule watu walikuwa na majonzi makubwa na wengi wao wakifikilia mstakabali wa taifa  lao la Tanzania.
 Wakati naianza safari yangu ya kuelekea Butiama baada ya miaka mingi kidogo kupita nikiwa njiani nikawa natafakari sana hivi Butiama ni sehemu ya namna gani? Amahakika ilikuwa ni safari ndefu sana  na nilifika Mwanza saa sita usiku na ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika mikoa ya kanda ya ziwa.
Na kwa muda wa siku mbili nilishinda Mwanza kwajili ya kupumnzika kutokana na uchovu wa safari ndefu na siku ya tatu nilianza safari kuelekea Mkoa wa Mara,nakumbuka nilipanda basi la kampuni ya Zakaria na ndani ya gari nilikaa na mama mmoja na wakati safari ikiendelea nikamuuliza mama huyo wewe ni mwenyeji wa mkoa wa Mara? Akanijibu ndiyo na je umewahi kufika Butiama kwa Mwalimu Nyerere akanijibu hapana.
Dah,nikaamua kukaa kimya kwa mshangao na sikumuuliza kitu tena,wakati safari inaendelea mara nikasikia kondakta kwa sauti ya ukali,Yule anayeelekea Butiama ashuke hapa,mara nikainuka haraka haraka  na kushuka.
Baada ya kushuka nikakutana na kundi la akina mama wakiuza bidhaa mbalimbali zikiwemo ndizi na vitu vingine ama hakika niliona ni akina mama wajasiliamali kwelikweli,nikalazimika kununua ndizi kwa mama mmoja kwa  lengo tu la kumuuliza nitafikaje Butiama? Bila ya hiyana akaniambia hapo niliposhuka ni kijiji cha Nyamisisi au Kayabakari akaniambia nipande tax (mchomoko) ambazo zilikuwa mbele yangu.
Baada ya abiria kujaa kwenye Tax tukaanza Safari,tukiwa njiani wakati dereva anadai Nauli akaniuliza unashuka wapi? Nikamwambia  kwa mwalimu Nyerere,mara akaniuliza tena wewe ni mgeni nikamwambia ndiyo,akaniuliza unatoka mkoa gani nikamwambia na baada ya muda mfupi akaniambia umeshafika na nikaamua kushuka.
Hakika baada ya kushuka nilishuhudia eneo hilo likiwa na utulivu wa hali ya juu sana ,na watu wachache wakipita na pembezoni nikashuhudia  ngedere wengi wasiowaogopa watu wakikatisha mitaa na kwa mbele nikawaona wazungu na watu wengine wakiwa kwenye lango  wakitoka na sehemu zingine nikaona  vilima vyenye mawe makubwa na miinuko na mabonde kiasi ya mashamba.
Baada ya kutembea kwa haraka haraka na kufika kwenye  lango kubwa lenye geti ,nikakalibishwa na dada mchangamfu na akaniambia nijiandikishe  kwenye daftali na kisha tukaingia ndani na kuanza kunieleza mambo mengi ambayo nilikuwa siyajui kabisa.
Akanionyesha kaburi la mwalimu na ndugu zake wengine ,vihenge  vya asili alivyokuwa anatumia mwalimu kuhifadhia nafaka,maktaba na nyumba yake ,magari aliyoyatumia  na na historia ndefu ya mwalimu akiwa kijijini Butiama pamoja na kunionyesha  maeneo mengine mengi  zaidi ambayo yalinifanya nijione mwenye bahati kubwa  kufika katika eneo la Mwitongo –Butiama  mkoani  Mara.
Nilipo maliza kutembelea eneo hilo alilokuwa anaishi mwalimu,ilinilazimu kwenda mtaani na kujionea maisha ya wananchi wa Butiama na kikubwa nilichostaajabishwa  ni maisha ya kawaida  kama yalivyo kwa wananchi wa maeneo mengine ya vijiji nchini Tanzania.
Na mara baada ya safari yangu nilianza safari ya kurudi Mwanza na kisha nikasafiri hadi Dar es salam na kufika eneo la Magomeni ambako kuna makumbusho ya Taifa juu ya maisha ya Mwalimu Nyerere,ikiwemo nyumba aliyoanzia maisha  na simulizi nyingine  nyingi kuhusu maisha ya mwalimu.
Tuvipende vitu vyetu kwanza mungu ibariki Tanzania.

Imeandaliwa na  Ng’oko Innocent

UJUMBE KWA FACEBOOK