TTCL

Habari

MAFUNZO YA UHASIBU (FFARS) YAINGIA SIKU YA PILI.

on

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya FFARS wakiwa kwenye vikundi wakifanya mazoezi ya kuandika miamala ya kifedha kwenye nyaraka na vitabu vya Uhasibu baada ya mafunzo ya darasani. Wahasibu walioshiriki mafunzo ya FFARS wakijadiliana mambo mbali mbali waliopata kwenye mafunzo.

MAFUNZO ya mfumo mpya wa Uhasibu na utoaji taarifa (Facility Financial Accounting and Reporting System) Kwa Wahasibu wa Sekta za Elimu na Afya kwa Halmashauri za Mikoa ya Nyanda za juu kusini yameingia katika siku ya pili jijini Mbeya.

Mafunzo hayo ambayo yanawahusisha Wahasibu kutoka Halmashauri za Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Katavi, Songwe na Rukwa katika Sekta za Elimu na Afya ambao wanatarajiwa kuwa wakufunzi katika Ngazi za Kata kwa shule za Msingi, Sekondari, Zahanati na vituo vya Afya.

Aidha katika siku ya kwanza washiriki walipatiwa mafunzo kwa kuelezwa maana halisi ya Mfumo mpya wa FFARS na kufundishwa mbinu za mfumo huo kabla ya kuanzishwa na baada ya kuanzishwa kwake.

Pia washiriki hao walipata nafasi ya kufundishwa mfumo wa manunuzi, maana na aina ya vitabu ya uhasibu, namna ya kuandaa na kuandika vitabu vya malipo, kupokelea fedha na uandikaji pamoja na namna ya kutoa hundi. Hata hivyo baadhi ya Washiriki wa mafunzo hayo walisema matarajio yao ni kwenda kuwafundisha Waimu na Wasimamizi wa Zahanati na Vituo vya Afya mfumo mpya wa kielekroniki wa Kihasibu ili kuleta uwajibikaji na nidhamu kwenye fedha.

Walisema asilimia kubwa ya watumishi katika ngazi za Kata na vijiji hawana uelewa kuhusu Uhasibu jambo ambalo linawapa ugumu wakati wa utoaji wa taarifa za fedha kwa wakaguzi hivyo baada ya kupata elimu itasaidia kuondoa mapungufu ambayo yalikuwa yakijitokeza.

Mkakati huo mpya wa kuboresha sekta ya afya ni msaada kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) kupitia mradi wa uimarishaji wa mifumo ya Sekta za umma(PS3) ambao umelenga katika sekta ya Afya,Elimu, Kilimo na Maji.

Aidha Mradi wa PS3 unatekelezwa kwa miaka mitano katika mikoa 13 ya Tanzania Bara ikilenga katika mifumo ya mawasiliano, Utawala bora na ushirikishwaji wananchi, Rasilimali watu na Fedha katika jamii zenye uhitaji.

UJUMBE KWA FACEBOOK