TTCL

Michezo

MIUNDOMBINU KIKWAZO CHA MICHEZO NCHINI

on

IMEELEZWA kuwa sekta ya michezo nchini inakabiliana na changamoto ya miundombinu duni na ukosefu wa vifaa vya michezo kwa Shule za Msingi.

Aidha imebainishwa kuwa  Shule mbalimbali wilayani Mbeya zimetajwa kuwa changamoto inayokwamisha jitihada za kuendeleza sekta ya michezo mashuleni ni kutokuwa na vifaa.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Katibu wa Kamati ya Mashindano ya Michezo ya wanafunzi wa Shule za msingi(Umitashumita) kata ya Igale,Mwalimu Atupakisye Jabir  alipokuwa akitoa taarifa ya hali ya michezo mashuleni kwenye uzinduzi wa mashindano hayo.

Mwalimu jabiri amesema miundombinu ya michezo ni duni na iliyopo haiko katika hali nzuri huku akisema pia vifaa vya michezo kama mipira,sare,nyavu,filimbi,saa za michezo na ngoma havitoshelezi.

Amesema pia kutokana na ukosefu wa usafiri kwaajili ya shughuli za michezo mashuleni,walimu na wanafunzi wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kwa miguu pale yanapoandaliwa mashindano au michezo ya kirafiki kati ya shule moja na nyingine au shule za kata moja na nyingine.

Amewasihi wadau mbalimbali kuona uwezekano wa kuzisaidia shule katika tasnia ya michezo kwakuwa mashuleni ndiko kuliko na msingi bora wa kuwapata wachezaji wazuri wanaoweza kuliwakilisha taifa katika mashindano mbalimbali kama inavyoonekana hivi sasa kwa timu ya Serengeti Boys ambayo sasa ni gumzo ndani nan je ya nchi.

Akifungua mashindano ya Umitashumita katika ngazi ya kata ya igale inayoshirikisha jumla ya shule tano za msingi,Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Usongwe lililopo Mbalizi Wilayani Mbeya,Idd Omary sambamba na kukabidhi msaada wa mipira mitano ameahidi kuendelea kushirikiana na shule zote wilayani hapa katika suala la michezo lengo likiwa ni kushiriki kuibua na kukuza vipaji vya michezo.

Omary amesema pamoja na faida nyinginezo lukuki za michezo,NMB inatambua kuwa nidhamu ya mtumishi yeyote kazini inatokana na msingi bora uliojengwa tangu angali mdogo hivyo kwa mwanafunzi kushiriki michezo ni sehemu ya kujifunza nidhamu bora.

Amewasihi wanafunzi kutoitumia fursa ya michezo kujiingiza katika masuala ya matumizi ya dawa za kulevya na ulevi kwakuwa kufanya hivyo kunaweza kuwasababishia kutofikia malengo yako kimichezo na hata kitaaluma.

Kwa upande wake Afisa Elimu Utamaduni wilaya ya Mbeya,Ashanuru Malange amesisitiza umuhimu wa Michezo mashuleni akisema Mwili wenye Afya huleta Akili yenye afya na ili afya ipatikane ni lazima mwili husika ufanye mazoezi.

Shule zinazounda mashindano ya Umitashumita katika kata ya Igale yatakayotoa timu kwaajili ya kushiriki mashindano hayo kwenye ngazi ya wilaya ni pamoja na shule ya msingi Igale,Izumbwe I,Shongo,Itaga na Horongo.

 

 

 

UJUMBE KWA FACEBOOK