TTCL

Makala

Mwandishi aibuka kitabu ‘Safari Hii Mwisho’

on

MWANDISHI Habari Christopher Nyenyembe 

Na,Mwandishi wetu

Mwandishi aibuka kitabu ‘Safari Hii Mwisho’

MWANDISHI Habari Christopher Nyenyembe ameibuka na kitabu chake alichotunga mwaka 1997 kilichoandikwa kwa jina la Safari hii Mwisho kikielezea mikakati na harakati za kupambana na vijana wanautumia dawa za kulevya na kufanya biashara hiyo haramu.

Mbeya yetu ilifanya mahojiano maalumu na Nyenyembe ambaye aliandika kitabu hicho takribani miaka 20 sasa tangu utawala wa serikali ya awamu ya tatu iliyoongozwa na,Rais mstaafu,Benjamin Mkapa na kuzinduliwa rasmi na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya Basil Mramba.

Nyenyembe alisema kuwa uamuzi wa kutunga kitabu hicho ilikuwa ni mchango wake wa awali kama mwandishi wa habari kutoa mchango wake wa kupiga vita biashara ya dawa za kulevya na matumizi yake ambayo yamekuwa yakiathiri kwa kiasi kikubwa nguvu kazi ya taifa ambao wengi ni vijana.

“Sikujua kabisa kuwa ndani ya miaka 20 yangeweza kuibuka kwa kasi yale niliyoyaandika katika kitabu changu cha ‘Safari hii mwisho’,nilikuwa na dhamira ya kweli kupitia kalamu ili kuiambia jamii kuwa utumiaji wa dawa za kulevya ni janga la dunia nzima lakini yale niliyoandika hayajaoza” alisema Nyenyembe.

Katika kitabu chake hicho chenye dibaji inayokielezea,alitoa ujumbe kuwa Safari hii mwisho ni kitabu chenye umbo halisi na mwelekeo wa dharuba kali iliyotumiwa na mwandishi ili kuwaasa vijana wa karne hii ya leo.Vijana ambao wanaendelea kuathiriwa na wimbi zito la uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya.

Aliendelea kuielezea hali hiyo kuwa ilitokana na mvuto wa pekee uliojitokeza wazi na kumfanya aandike hayo ili jamii nzima iweze kutambua ni nini kinachoweza kuthaminiwa na umma.Ni mali mbele au Taifa lenye jamii taahira.

Dibaji yake ilibeba ujumbe mzito ikijibu swali hilo na kudai kuwa ndio msingi madhubuti uliomfanya awe makini katika kukiandika kitabu hicho na ni mategemeo yake kuwa ‘Safari Hii Mwisho’ ndio wosia wake kwa wale wote wanaojihusisha kikamilifu bila woga na biashara haramu ya uuzaji na utumiaji wa madawa ya kulevya.

” Aliyeniamsha upya na kuanza kupekua kwenye kabati ili kupata angalau nakala moja ya kitabu changu ni Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam,Paulo Makonda,tatizo nililoligundua ni namna alivyotumia njia za kuwataja hadharani wale wote aliowatuhumu,kutumia,kusambaza na kuingiza madawa hayo,nia na dhamira ni njema isipokuwa mbinu zilizotumiwa ni dhaifu” alisema Nyenyembe.

Alisema kuwa anatambua msimamo thabiti wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ya kupambana na vitendo vyote vya uhalifu,matumizi ya dawa za kulevya,ufisadi,rushwa,watumishi hewa na ajira hewa lakini mambo yote hayo hufanikiwa na kiwango kikubwa endapo utawala wa kisheria unatamalaki bila kuathiri katiba ya nchi na mfumo wa utawala bora.

Kwamba anaamini kuwa kwa vile Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam ameamua kujitoa kimasomaso bado ana changamoto kubwa ya kujua na kuwatambua marafiki wa kweli wanaoweza kumsaidia kwani ana hofu kubwa kuwa watoa taarifa wengine nao hawako safi wanafanya mambio hayo kwa magomvi yao na kukomoana ama kisiasa au kiuchumi hivyo alimtahadharisha kuwa makini.

“Nampongeza Rais Magufuli kwa kumteua Kamishina Sianga kuongoza mamlaka ya kupambana na madawa ya kulevya,hilo ni jukumu la watanzania wote kujua wajibu wetu na naamini yeyote aliyebahatika kukisoma kitabu changu chenye kurasa 47 niligusia wahusika na mbinu za unasaji,huo ndio mchango wangu na nitaona kama inafaa zaidi kueleza maudhui ya kitabu changu hicho” alisema Nyenyembe.

Nyenyembe akiwa Mwandishi wa habari Mwandamizi vile vile amebahatika kutunukiwa mara mbili tuzo za uandishi wa habari za uchunguzi mwaka 2007 na 2008 hali inayoonyesha kuwa ni mbobevu katika uandishi wa habari za uchunguzi na kitabu chake hicho pia kilifanyiwa uchambuzi miaka iliyopita na magazeti ya hapa nchini.

mwisho.

UJUMBE KWA FACEBOOK