TTCL

Habari

MWENENDO WA KESI YA SUGU KABLA YA KUANZA KUJITETEA FEBRUARI 8, 2018.

on

MBUNGE wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi (Sugu) pamoja na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Mbeya wakikabiliwa na kosa la matumizi ya lugha ya fedha dhidi ya Rais Dk. Magufuli.

Watuhumiwa hao walifikishwa Mahakamani hapo Januari 16, mwaka huu na kusomewa Mashtaka yanayowakabili kisha kesi hiyo kuahirishwa  hadi Januari 19 mwaka huu kwa washtakiwa kurudishwa rumande baada ya kukosa  dhamana.

Akiwasomea Shtaka linalowakabiri katika Kesi hiyo yenye namba 12/2018 Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Joseph Pande ambaye ni Wakili Mkuu wa Serikali akisaidiwa na Baraka Mgaya pamoja na Othman Mtenga wakati watuhumiwa wanatetewa na wakili Msomi Boniphace Mwabukusi akisaidiwa na Wakili Hekima Mwasiku pamoja na Sabina Yongo alisema  walitenda kosa hilo 30 Disemba, 2017 katika kiwanja cha Shule ya msingi Mwenge iliyopo katika Kata ya Ruanda jijini Mbeya.

Baada ya kesi hiyo kutajwa na watuhumiwa kukana shitaka, Hakimu alisema  dhamana iko wazi kwa watuhumiwa ndipo wakili wa serikali akaiambia Mahakama iwaweke ndani watuhumiwa kwa ajili ya usalama wao na kwamba  walikuwa wakifuatiliwa na kuna viashiria vya usalama wao kuwa mdogo.

Mwanasheria huyo aliongeza kuwa  sababu nyingine ni kwamba Mbunge Mbilinyi alikiuka masharti kwa kutoripoti Januari 15, 2018  kwenye Ofisi za polisi Mkoa wa Mbeya kama alivyotakiwa.

Hata hivyo upande wa Mashtaka ukataka kuwasilisha Barua ya kibali cha Mbunge huyo kufanya Mkutano wa Hadahara kutoka kwa Kamanda wa Polisi ukatolewa lakini ubishani ukapelekea Hakimu kuamuru kuahirisha kesi hiyo na kwamba atatoa uamuzi wa dhamana hiyo Januari 19, 2018 kutokana na wafanyakazi wa mahakama waliopaswa kuandika rulling kutokuwepo mahakamani hapo.

Katika maelezo ya awali ilielezwa kuwa baada ya  Mkutano huo Mbunge huyo pamoja na Katibu waliitwa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya Januari 2, 2018 na kuhojiwa pamoja na kuchukuliwa maelezo na baada ya hapo waliripoti mara kadhaa kabla ya kufikishwa mahakamani.

Januari 19, mwaka huu Kesi namba 12/2018 inayomhusu Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi na Emmanuel Masonga Katibu CHADEMA Kanda ya Nyasa wanayotuhumumiwa kumfedhehesha Rais ilianza kusikilizwa  mbele ya Hakimu Mfawidhi Michael Mteite.

Upande wa mashitaka ukiongozwa na Joseph Pande Wakili Mkuu wa Serikali akisaidiwa na Baraka Mgaya pamoja na Othman Mtenga wakati watuhumiwa wanatetewa na wakili Boniphace Mwabukusi akisaidiwa na Wakili Hekima Mwasiku pamoja na Sabina Yongo.

Mashahidi watatu wa upande wa mashitaka walianza kutoa ushahidi wao akiwemo Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbeya mjini Keneth James Chacha,Boniphace Mwaitolola(34)mkazi wa Soweto jijini Mbeya na Afisa Upelelezi William Nyamakomage kutoka ofisi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya.

Shahidi wa kwanza aliiambia Mahakama kuwa alipata barua ya taarifa ya mkutano Disemba 27 mwaka jana na kuidhinisha Disemba 29 na mkutano kuruhusiwa kufanyika Disemba 30 mwaka jana ambapo pia taarifa zilitolewa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC),Afisa Upelelezi Mkoa (RCO),Afisa usalama wa Taifa Wilaya ya Mbeya na Mkuu wa Wilaya.

Aliendelea  kutoa maelezo kuwa alimwambia kuwa katika mkutano wa Mbunge yasiwepo matusi wala kuitukana Serikali.

Hata hivyo James Chacha alisema alipata taarifa kutoka kwa walinzi wa usalama juu ya watuhumiwa kumtukana Rais ambapo  Chacha aliwasilisha barua zote kama kielelezo ambazo zote zilipokelewa kama ushahidi na kuandikwa kama kielelezo namba moja.

Kwa upande wake Shahidi wa pili Boniphace Mwaitolola aliiambia Mahakama kuwa alikuwepo eneo la mkutano na kwamba aliwasikia watuhumiwa wakitukana hali iliyomchukiza kwa kutukanwa Rais.

Kesi iliahirishwa baada ya saa moja ambapo upande wa mashitaka utaleta mashahidi wengine.Hata hivyo baada ya ahirisho la muda Afisa Upelelezi kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi William Nyamakomage  aliiambia Mahakama kuwa Disemba 30 mwaka jana alipata taarifa kutoka kwa RCO ASP Modestus Chambo kwenda katika mkutano uliopangwa kufanyika siku hiyo viwanja vya shule ya msingi Mwenge.

Alisema alifika saa 10:30-10:45 jioni ambapo akiwa mita thelathini au zaidi ya hapo aliwasikia Mbunge Joseph Mbilinyi na Katibu Emmanuel Masonga wakitoa maneno ya kumfedhehesha Rais John Pombe Magufuli kama watu wengi wanauawa, wengine wanatupwa kwenye viroba na wengine kutekwa kama Roma, Benn Saanane pia mheshimiwa Sugu kuzuiwa kuongea.

Baada ya kusikilizwa kwa mashahidi hao Hakimu Michael Mteite aliahirisha kesi hadi Januari 23 mwaka huu upande wa mashitaka utakapoleta mashahidi wengine ambapo Mbunge na Katibu walipelekwa mahabusu ya Gereza la Ruanda.

Januari 23, mwaka huu Kesi inayowakabili Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyasa Emmanuel Masonga ya tuhuma za kumfedhehesha Rais ilishindwa kuendelea baada ya kuibuka kwa ubishani mkubwa.

Kesi hiyo iliahirishwa  baada ya kutokea ubishani wa kisheria baada ya shahidi wa tano Inspector Joram Magova upande wa mashitaka kumaliza kutoa ushahidi wake na Wakili Mkuu wa Serikali Joseph Pande kuiomba mahakama isikilize video na sauti za watuhumiwa walipokuwa wakihutubia Disemba 30 mwaka jana.

Mapema asubuhi shahidi wa nne upande wa Serikali Sajenti Daniel Masanja Askari Polisi mwenye namba F 679 mtunza vielelezo ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya akiongozwa na Mawakili Joseph Pande, Ofmed Mtenga na Baraka Mgaya, aliambia mahakama alipokea tape recorder kutoka kwa Inspector Joram Magova ambaye ni mkuu wa kitengo cha Tehama ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Mbeya Disemba 30 mwaka jana.

Alisema alipokea recoder hiyo namba 158 yenye rangi ya fedha na kuisajili katika kitabu cha kumbukumbu kisha kuifungia kwenye kasiki.

Alisema Januari 2 mwaka huu aliombwa na Inspector Joram kwa ajili ya kuwasikilizisha Mbunge na Katibu katika chumba cha mikutano ofisi ya Kamanda wa Polisi.

Wakili wa utetezi Boniphace Mwabukusi na Hekima Mwasipu waliiomba Mahakama kutopokea vielelezo kwa kuwa hakuwepo eneo la tukio na recorder hiyo inaweza kuchezewa.

Hakimu Michael Mteite aliahirisha kwa muda shauri hilo ambapo baada ya muda alitoa uamuzi wa kupokelewa vielelezo hivyo na kuwa kielelezo cha pili.

Shahidi wa tano Inspector Joram Magova aliiambia mahakama kuwa alifika eneo la mkutano majira ya saa kumi na moja jioni na kusikiliza mkutano huo ambapo alianza Katibu Emmanuel Masonga kwa kutoa kauli kuwa “watu wanauawa kweupe, wanatekwa mchana kweupe, Watanzania wanauawa na kutupwa kwenye viroba, Rais wetu Magufuli ameona njia pekee ya kuwatawala Watanzania ni kuwaua “.

Joram aliendelea kusema  kuwa baada ya Katibu kumaliza alimkaribisha Mbunge Joseph Mbilinyi ambaye alianza kuelezea shughuli za maendeleo baadae alikazia maneno ya Katibu kwa kusema “hayo ndiyo mambo ambayo Magufuli anataka kupendwa.

Alisema Sugu aliendelea kuhubiri kuwa Rais  hawezi kupendwa kwa Lema kuwekwa ndani kwa miezi minne, hawezi kupendwa kwa kumteka Roma  na Benn Saanane ambaye hajaoneka mpaka leo “.

Kutokana na ushahidi huo Wakili wa Serikali Joseph Pande aliiomba mahakama isikilize sauti hizo za watuhumiwa ndani ya mahakama, Hoja ambayo  ilipingwa na Wakili Mwabukusi akinukuu kifungu cha sheria ya mitandao namba 18  (3)(b) ya mwaka 2015 na 18 (2)(a)(b) ya mwaka 2015.

Upande wa Serikali ukitetea hoja yake kwa kifungu 18,19 na 20 pia sheria ya ushahidi na 59 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Baada ya mabishano ya kisheria ya Mawakili hao Hakimu Michael Mteite aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 24 mwaka huu atakapotoa uamuzi wa sauti isikilizwe au la.

Watuhumiwa wamerudishwa  mahabusu.

Januari 24, mwaka huu kesi iliendelea tena kwa Hakimu Mteite kuruhusu Mahakama kusikiliza ushahidi wa Sauti na video ambao ulisikilizwa mahakamani hapo kisha Upande wa Mashtaka ukasema umefunga ushahidi.

Awali upande wa mashtaka ulidai utakuwa na mashahidi saba lakini ulifunga ushahidi kwa mashahidi watano na kuongeza kuwa hawaoni haja ya kuongezea ushahidi mwingine baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na shahidi namba tano.

Kwa upande wa utetezi ulisema unao mashahidi 7 na vielelezo nane lakini kabla ya hapo Wakili wa utetezi alisema washtakiwa wana neno la kusema ambapo Hakimu aliwaruhusu kuongea.

Baada ya kuruhusiwa Washtakiwa hao, Joseph Mbilinyi (Sugu) alisema hana imani na Hakimu anayeendesha kesi hiyo kutokana na sababu tatu kwa kile alichodai Hakimu ameegemea upande mmoja na kumyima dhamana kinyume cha sheria.

Sugu alitaja sababu nyingine kuwa uamuzi wa Hakimu kupokea Rekoda kama kielelezo pamoja na kukiri mbele ya Mawakili kuwa kesi hiyo inampa shida hivyo kuonekana kama anashinikizwa.

Naye mshtakiwa Emmanuel Masonga alisema pia hana imani na Hakimu kutokana na uamuzi wake wa kupokea vielelezo, kuwanyima dhamana na kukiri kwa Hakimu kuwa kesi hiyo inampa shida.

Kutokana na hoja hizo, Hakimu aliahirisha kesi hiyo kwa muda wa saa  moja ambapo baada ya kurejea alisema hakubaliani na hoja iliyotolewa na washtakiwa za kumkataa hivyo ataendelea na kesi hiyo kwani hana maslahi nayo pia alikula kiapo cha kusimamia haki.

Hata hivyo baada ya ombi lao la kumkataa Hakimu  kugonga mwamba Mawakili wa Utetezi walisema hawatakuwa tayari kuendelea na kesi hiyo hivyo Washtakiwa wanaweza kujitetea wenyewe au kutafuta mawakili wengine.

Mshtakiwa Sugu aliiomba Mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa muda wa wiki mbili ili waweze kutafuta mawakili wengine hoja ambayo haikupingwa na upande wa mashtaka hivyo kesi ikaahirishwa hadi Februari 8 mwaka huu watakapoanza kujitetea.

Nje ya Mahakama Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe aliwasihi wafuasi wa chama hicho kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho Chama kinajipanga kuongeza nguvu ya mawakili ili kumtetea Mbunge wake.

UJUMBE KWA FACEBOOK