TTCL

Habari

RC MAKALA ATAKA WANANCHI WAPATIWE TAARIFA YA REA

on

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla akihutubia moja ya mikutano iliyofanyika mkoani Mbeya.

MKUU wa  mkoa wa Mbeya,Amos Makalla ametoa muda wa juma moja kwa Halmashauri ya wilaya ya Rungwe na Halmashauri ya Busokelo kuandaa mikutano ya wenyeviti wa vijiji ili kuwapa mchanganuo wa utekelezaji wa mradi wa Umeme kupitia wakala wa Umeme vijijini(Rea).

Makalla ametoa agizo hilo  kwenye mkutano wa kusikiliza Kero za wananchi uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Tukuyu kilichopo Msasani wilayani Rungwe.

Makalla amelazimika kuyasema hayo kufuatia malalamiko mengi yaliyowasilishwa na wananchi kwenye mkutano huo mengi yakionesha wananchi kuwa na uelewa mdogo juu ya utekelezaji wa mradi wa Rea.

Kutokana na uelewa huo mdogo baadhi ya wananchi wamekuwa wakitapeliwa na watu wanaoiitwa vishoka huku wengine pia wakibaki wakilaumu kuofikiwa na mradi au vijiji vyao kurukwa wakati havikuwa katika awamu zilizopita za Rea.

Makalla amesema wenyeviti wa vijiji wanapasawa kupewa uelewa wa mradi husika ili na wao waende kuwaelimisha wananchi wao ili kusiwepo na sintofahamu tena juu ya mradi husika.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Rungwe,Chalya Julius amesema malalamiko ya wananchi juu ya utekelezwaji wa mradi wa Rea ni mengi na mara nyingi watu wamekuwa wakifika ofisini kwake kuwasilisha kero hizo.

Amesema licha ya mradi kuingiliwa na matapeli pia kumekuwepo na malalamiko ya Mradi kutozifikia taasisi za kiserikali hususani Shule na Zahanati jambo linaloonekana ni ukiukwaji wa maelekezo ya Serikali kwenye mradi huo.

Awali akiwasilisha kero mmoja wa wakazi wa kijiji cha Syukula kata ya Kyimo wilayani hapa,Timoth Kaswaga amesema wananchi wa kijiji hicho wanahitaji umeme wenye nguvu ya kutosha kwakuwa wanatarajia kujiunga katika vikundi ili waweze kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani kwenye mazao kabla ya kuyauza.

UJUMBE KWA FACEBOOK