TTCL

Habari

SAE PIPELINE VICOBA YA JIJINI MBEYA YAWAKUMBUKA VIJANA WA MAJUMBANI

on

Mratibu wa Jinsia na watoto kutoka Shirika la Caritas chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya, Praxeda Manyuke akitoa somo la kujitambua kwa Vijana wa majumbani katika hafla iliyoandaliwa na akina mama wa Sae Pipeline Vicoba.Balozi wa Mtaa wa Pipeline Sae, Mariam Kabuje  akitoa somo la kujitambua kwa Vijana wa majumbani katika hafla iliyoandaliwa na akina mama wa Sae Pipeline Vicoba. Mwanachama wa Vicoba, Furahia Miho akitoa somo la kujitambua kwa Vijana wa majumbani katika hafla iliyoandaliwa na akina mama wa Sae Pipeline Vicoba. Mratibu wa Jinsia na watoto kutoka Shirika la Caritas chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya, Praxeda Manyuke akimpa zawadi ya Kanga mmoja wa vijana ambao ni Watumishi wa  majumbani katika hafla iliyoandaliwa na akina mama wa Sae Pipeline Vicoba. Mratibu wa Jinsia na watoto kutoka Shirika la Caritas chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya, Praxeda Manyuke akimpa zawadi ya Tshirt mmoja wa vijana ambao ni Watumishi wa  majumbani katika hafla iliyoandaliwa na akina mama wa Sae Pipeline Vicoba. Baadhi ya Vijana ambao ni watumishi wa majumbani wakifuatilia semina inayotolewa kwao Baadhi ya Wanachama wa Kikoba cha Sae Pipeline  wakifurahia jambo katika semina kwa vijana wanaoishi majumbaniWanachama wa Vicoba pamoja na Vijana waishio majumbani wakifuatilia kwa makini masomo yanayotolewa na wawezeshaji (hawapo pichani)

 

VIJANA wanaofanya kazi majumbani wa kike na kiume wameiomba jamii hususani Walezi na waajiri wao kuwapa huduma za msingi kama vile upendo, amani, Mshikamano pamoja na stahiki zao ili nao wafurahie maisha kama watoto wengine.

 

Vijana hao walitoa rai hiyo jana katika Hafla ya kupewa elimu pamoja na zawadi kutoka kwenye Kikundi cha kuweka na kukopa cha Vicoba  Sae Pipeline kilichopo Sae jijini Mbeya ambapo mbali na Zawadi za nguo pia walipewa Elimu ya kujitambua na namna ya kuishi na Walezi wao.

 

Vijana hao wapatao 55 kutoka katika Kaya mbalimbali za Mtaa wa Pipeline wakiwemo Wasichana 35 na Wavulana 20 wanaofanya kazi za majumbani ambao walitambuliwa na Kikoba hicho walisema matarajio yao katika kazi hizo ni kupata ushirikiano na kuthaminiwa na Waajiri wao.

 

Akitoa somo kwa vijana hao, Mtaribu wa Jinsia na Watoto kutoka Shirika la Caritas chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya,Praxeda Manyuke alisema Vijana wanapaswa kujitambua katika jamii wanayoishi ili kujua walipo wapo kwa ajili gani na nini malengo yao ya baadae.

 

Aidha alitoa wito kwa Walezi kuwa wanapaswa kuwachukulia vijana hao kama moja ya familia zao kwani wao wanakua ni mbadala ya Wazazi wao hivyo ni wajibu kwa kijana kumheshimu na kutimiza wajibu wake sambamba na Mlezi kumtimizia mahitaji yake ya msingi kama watoto wengine.

 

“Ni waombe Walezi wenzangu tunapaswa kuwaona hawa watoto kama wetu sio lazima Mtoto akitoka getini kila mtu ajue ni Housegirl au house boy mvalishe vizuri ikiwezekana wavae sare na watoto wenu na mkifanya hivyo mtakaa nao kwa muda mrefu sana” alisema Mwezeshaji huyo.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikoba hicho, Zaina Abubakari alisema Vicoba vilianzishwa mwezi Machi mwaka huu na Wanawake 30 lengo likiwa ni kusaidiana na kuwezeshana lakini baadaye wakaamua kusaidia jamii ambayo imesahaulika ambayo ni watumishi wa majumbani.

 

Alisema matarajio ya mbeleni ni kupita kila Kaya hadi maeneo ya vijijini kuwatambua vijana hao na kuwapatia misaada mbalimbali ikiwemo Elimu ya kujitambua kama kijana ikiwemo namna ya kujikinga na magonjwa mbalimbali hususani magonjwa yanayotokana na ngono zembe.

 

Naye Balozi wa Mtaa wa Pipeline, Mariam Kabuje,aliwaasa Walezi kuwalipa stahiki zao vijana wao kwa wakati ili kuwaondolea manung’uniko yasiyokuwa ya lazima na hatimaye kupelekea kuwa na tabia mbaya ikiwemo unyanyasaji dhidi ya Watoto pamoja na wizi.

 

“Kwanza niwaambie vijana wangu usipolipwa mshahara nenda kashtaki kwa mzee yeyote au njoo kwangu kama balozi vinginevyo usilipize kwa kuiba au kumtesa mtoto unaemlea yeye hana kosa mwenye kosa ni bosi wako, nanyi Walezi walipeni hawa vijana stahiki zao kwa wakati mtaishi nao vizuri na mtajipatie heshima” alisema Balozi.

 

UJUMBE KWA FACEBOOK