TTCL

Habari

SERIKALI ZA MITAA KUTUMIA MFUMO MMOJA WA UHASIBU (EPICOR 10.2).

on

Afisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Paulina Ndigeza akifungua mafunzo ya Epicor kwa Wahasibu na Watunza hazina wa Mikoa ya Mbeya, Songwe na Katavi  kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja yanayofanyika Usungilo jijini Mbeya. Afisa Msimamizi wa Fedha kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, Mmaka Mwinjaka akielezea umuhimu wa mafunzo ya Epicor 10.2 kwa Wahasibu na Watunza hazina. Mkuu wa mfumo wa Mawasiliano kutoka Mradi wa uimarishaji wa mifumo ya sekta za umma (PS3) Desideri Wengaa akielezea umuhimu na malengo ya mfumo wa Epicor katika uimarishaji wa sekta za fedha.  Baadhi ya Washiriki na Maafisa wa PS3 wakifuatilia uwasilishwaji wa mada kuhusu mafunzo ya EPICOR 10.2 kwa Wahasibu na Watunza hazina.

Wahasibu na Watunza hazina wa Halmashauri za Mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa wakiwa katika chumba cha mafunzo Baadhi ya Wahasibu na Watunza hazina wa Halmashauri za Mikoa ya Mbeya, Rukwa na Songwe wakifuatilia kwa makini mafunzo ya Epicor 10.2 Washiriki wa Mafunzo ya Epicor 10.2 katika kituo cha Mbeya wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi baada ya kufungua rasmi.

 

 

MAMLAKA zote za Serikali za Mitaa nchini Tanzania zinatarajia kuanza kutumia mfumo mmoja wa uhasibu ujilikanao kama Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma, tolea la 10.2 (Epicor10.2), utakaosaidia kuhakikisha kuna mfanano katika uhasibu, utoaji taarifa na usimamizi wa fedha.

 

Aidha mfumo huo unatajiwa kuanza kutumika  Julai 1, mwaka huu, kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa 185 za Tanzania bara, uliowezeshwa kwa msaada wa Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).

 

Akizungumza wakati wa mafunzo kwa Wahasibu na Waweka Hazina wa Halmashauri za Mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa yanayoendelea katika ukumbi wa Hoteli ya Usungilo jijini Mbeya, Mku wa Mfumo wa Mawasiliano wa PS3, Desderi Wengaa alisema uzinduzi wa mfumo huo mpya utafuatiwa na mafunzo ya kina ya wiki tatu kwa watumishi.

 

Alisema Watumishi  950 na wale wa kada za uhasibu kutoka katika Mamlaka zote za Serikali za Mitaa 185 za Tanzania bara kuanzia Juni 4, mwaka huu watanufaika na mafunzo hayo.

 

Alisema Mafunzo hayo yataendeshwa na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Serikali ya Marekani kupitia Mradi wa USAID wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).  Mafunzo yatafanyika katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Mtwara, Mbeya, Kagera na Mwanza.

 

“Moja kati ya maboresha makubwa katika mfumo mpya wa usimamizi wa fedha za umma ni kushushwa kwa mfumo hadi kwenye ngazi ya mtoa huduma,  Kwa sasa matumizi yote yanayofanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa vituo vyake vya afya na shule yatahifadhiwa na kuwekwa wazi kwa vituo vya kutolea huduma pamoja na jamii wanayoitumikia” alisema Afisa huyo.

 

Aliongeza kuwa Maboresho mengine katika mfumo wa usimamizi wa fedha za umma katika tolea la 10.2 (Epicor 10.2) ni kwamba mifumo yote ya msingi ya usimamizi wa fedha katika sekta za umma kwa sasa itaweza kuwasiliana na kushirikishana taarifa.

 

Alisema Matoleo yaliyopita ya mfumo wa usimamizi wa fedha za umma yalijumuisha hitilafu za kiufundi ambazo zilididimiza mbinu bora za uhasibu na taratibu za usimamizi wa fedha, na kusababisha kuwepo kwa hati chafu kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

 

Alisema mfumo wa Epicor 10.2 utaunganishwa na mfumo unaowezesha mabenki kulipana Tanzania (TISS) ambao utaruhusu malipo yote kufanyika kwa njia ya kielektroniki, pia unahusisha Muundo mpya wa uhasibu (New Chart of Account) pamoja na Kasma Mpya ya 2014 (GFS) kama ilivyoelekezwa na Wizara ya Fedha na Mipango.

 

Awali akifungua mafunzo hayo, Afisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Paulina Ndigeza akimwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja aliwapongeza waandaaji wa mafunzo kwa kufanikisha utengenezaji wa mfumo huo.

 

 

 

Alisema Mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo ili waweze kusimamia mapato na matumizi ya Fedha za Umma kwenye Halmashauri na pia kuwapatia uelewa wa mabadiliko ya msingi yalilofanyika bila kukwamisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Aliongeza kuwa Mafunzo hayo yataondoa changamoto za utoaji wa taarifa hasa kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma pamoja na kuunganisha taarifa hizo kwenye Hesabu za Halmashauri, pia utatoa taarifa za utekelezaji za mipango na bajeti kwa kuzingatia matumizi ya fedha yaliyofanyika.

 

Alisema  matumizi ya mfumo wa Epicor toleo la 10.2 ni hatua kubwa katika utekelezaji wa dhana nzima ya uwazi, uwajibikaji na utawala bora katika usimamizi wa Fedha za umma.

 

“Naomba niwapongeze wataalam wote walioshiriki kufanikisha mifumo yetu ya LGRCIS (Mfumo wa Mapato), PlanRep, FFARS na Epicor kuweza kubadilishana taarifa. Pia, naomba nichukue fursa hii kuwashukuru sana Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) kupitia mradi wa PS3 kwa kufadhili mafunzo haya, maana wamekuwa wanafanya kazi kwa karibu sana na Serikali ya Tanzania” alisema  na kuongeza.

 

“Sisi Makatibu Tawala wa Mikoa, ambao ni viongozi wa Mikoa tutahakikisha matumizi sahihi ya mifumo yanakuwepo ikiwemo matumizi ya taarifa katika kufanya maamuzi kuanzia ngazi za vituo vya kutoa huduma mpaka ngazi ya Mkoa” alisema Katibu Tawala.

 

Aliongeza kuwa Uwekezaji mkubwa uliofanyika katika usanifu na uandaaji wa mifumo hiyo ni lazima ienziwe kwa kuhakikisha adhma inafikiwa na kila mmoja katika sehemu anayofanyia kazi anawajibika ipasavyo.

UJUMBE KWA FACEBOOK