TTCL

Habari

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 05.02.2018.

on

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga akiwaonesha Waandishi wa Habari baadhi ya vitu vilivyokutwa kwa Majambazi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga akizungumza na waandishi wa habari Mtuhumiwa wa wizi wa mtoto akiwa katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya baada ya kukamatwa Mali za wizi zilizokutwa kwa majambazi baada ya msako Watuhumiwa wa ujambazi wakiwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi.

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 05.02.2018.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu ili kuhakikisha kuwa wageni na wakazi wa Mkoa huu wanaendelea kuwa salama na mali zao. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa usalama na kufanikiwa kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kukamata watuhumiwa watatu wa matukio mawili tofauti katika Wilaya ya Mbeya na Chunya.

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA UJAMBAZI WAKIWA NA SILAHA MBALIMBALI.

Mnamo tarehe 02 Februari, 2018 majira ya saa 20:00 usiku huko katika Kitongoji cha Kasanga – Kanyika, Kijiji cha Lupa – Market, Kata ya Kasanga, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanikiwa kuwakamata majambazi wawili ambao wamefahamika kwa majina ya 1. FITINA RUBEN mwanamume [30] na 2. SUMBUKO SANGA mwanamume [32] wote wakazi wa Chunya mjini.

Baada ya kukamatwa na kufanyiwa upekuzi, watuhumiwa hao wa tukio la ujambazi walikutwa na silaha na vitu mbalimbali ambavyo huvitumia katika uhalifu. Silaha/Vitu hivyo ni:-

 1. Bunduki moja aina ya short gun iliyotengenezwa kienyeji.
 2. Risasi moja inayotumiwa na silaha aina ya short gun.
 3. Manati moja.
 4. Maski Tatu
 5. Rungu moja
 6. Panga moja
 7. Nondo moja
 8. Banio moja (praise)
 9. Koti moja la kijeshi.
 10. Gloves moja.
 11. Mzula mmoja na
 12. Simu moja aina ya Tecno ambayo mmiliki wake bado hajafahamika.

Awali mnamo tarehe 31 Januari,2018 majira ya saa 15:00 Alasiri huko katika Kitongoji cha Kasanga – Kanyika, Kijiji cha Lupa – Market, Kata ya Kasanga, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya  Chunya, Mkoa wa Mbeya, Mfanyabiashara wa Madini anayefahamika kwa jina la MWILE SINJALE mwanamume [40] Mkazi wa Kasanga – Kanyika aliuawa kwa kupigwa risasi moja kichwani kwa kutumia silaha/bunduki aina ya Shot gun na watu wanne wanaume ambao waliokuwa na bunduki hiyo na mapanga 3 huku nyuso zao wakizifunika kwa mask ambao baada ya tukio hilo watu hao walifanikiwa kutokomea porini/msituni.

Aidha marehemu alikuwa akitokea Chunya mjini kwa kutumia usafiri wa pikipiki yake akiwa amepakiwa na mfanyakazi wake na alikuwa amebeba  mikate mikubwa miwili kwenye Lasket ya mgongoni, hivyo watu hao walidhani amebeba pesa na kisha kumvamia na kumuua.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali na kufanikiwa kuwakamata majambazi wawili kati ya wanne ambao inadaiwa kuhusika katika tukio hilo la tarehe 31 Januari, 2018. Baada ya mahojiano, watuhumiwa wamekiri kuhusika na mauaji ya mfanyabiashara huyo wa madini. Upelelezi unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwasaka watuhumiwa wengine wawili waliohusika katika tukio hilo la mauaji ya Mfanyabiashara huyo.

KUPATIKANA KWA MTUHUMIWA WA WIZI WA MTOTO.

 Mnamo tarehe 03 Februari, 2018 majira ya saa 12:00 Mchana huko maeneo ya mtaa wa Mponja – Uyole, Kata ya Igawilo, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Viongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya walifanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la HAPPY CHARLES [24] Mama Lishe, Mkazi wa Airport ya Zamani akiwa na mtoto mchanga jinsia ya kike aliyemuiba Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.

Awali mnamo tarehe 01 Februari, 2018 majira ya saa 04:00 usiku huko katika wodi ya watoto Hospitali ya Mkoa wa Mbeya iliyopo Kata ya Forest Mpya, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya, mwanamke mmoja anayefahamika kwa jina la SARAH MWASANGA [35] Mkazi wa Iganzo akiwa katika wodi ya wazazi Hospitalini hapo baada ya kujifungua mtoto wa kike aligundua kuibiwa kwa mtoto huyo na mtu asiyefahamika.

Kutokana na tukio hilo, uongozi wa Hospitali hiyo ulitoa taarifa kituo kikuu cha Polisi [Central] na ndipo upelelezi kuhusiana na tukio hilo ulianza kufanyika. Taarifa za siri zilipatikana na kubainisha kuwa huko maeneo ya Airport ya zamani kuna mama mmoja aitwaye HAPPY CHARLES [24] Mkazi wa Airport ambaye hapo awali alikuwa akimdanganya mume wake aitwaye CHILUBA PETER, Dereva Taxi Hospitali ya Rufaa Mbeya na Mkazi wa Airport kuwa ni mjamzito na kwamba amejifungua mtoto wa kike tarehe 31 Februari, 2018 na ndipo ufuatiliaji wa kuwapata watu hao ulianza.

Mtuhumiwa alikamatwa akiwa maeneo ya mtaa wa mponja – uyole, kata ya igawilo, tarafa ya iyunga kwa mama yake mzazi aitwaye MARY AKIMU [59] Mkazi wa Mtaa wa Mponja – Uyole ambapo alikwenda kwa ajili ya kupata huduma za uzazi. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

WITO:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA anatoa wito kwa jamii kuondokana na tamaa ya kutaka utajiri kwa njia zisizo halali kwa kujihusisha na uhalifu na badala yake watafute shughuli halali kwa ajili ya kujipatia kipato. Aidha anatoa onyo kali kwa yeyote atakayejihusisha na uhalifu kuwa Jeshi la Polisi halitakuwa na huruma na kuhakikisha anakamatwa na kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria. Pia Kamanda MPINGA anatoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia uhalifu ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za mtu/watu au kikundi cha watu wanachokitilia mashaka ili upelelezi ufanyike dhidi yao.

UJUMBE KWA FACEBOOK