TTCL

Habari

UBALOZI WA POLLAND WACHANGIA VIFAA VYA ELIMU NA AFYA ILUNGU MBEYA DC

on

Kaimu Balozi wa Poland nchini Tanzania Dk. Ewelina Lubieniecka akikabidhi msaada wa vifaa tiba kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Ilungu  kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Amelchiory Kulwizila kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla katika hafla iliyofanyika katika Kijiji cha Ifupa Kata ya Ilungu Wilaya ya Mbeya mkoani hapa. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Amelchiory Kulwizila na Mganga mkuu wa Wilaya ya Mbeya Dk.Louis Chomboko wakionesha baadhi ya vifaa tiba walivyopokea kutoka kwa Balozi wa Poland kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla katika hafla iliyofanyika katika Kijiji cha Ifupa Kata ya Ilungu Wilaya ya Mbeya mkoani hapa. Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ilungu, Daudi Cholobi akionesha baadhi ya vifaa vilivyotolewa na Ubalozi wa Polland kwa ajili ya wanafunzi wa Bweni baada ya kukabidhiwa rasmi na Kaimu Balozi wa Poland nchini Tanzania.

 

UBALOZI wa Poland nchini Tanzania umetoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 139 za Kitanzania kwenye Sekta za afya na Elimu katika Kata ya Ilungu Wilaya ya Mbeya mkoani hapa.

 

Msaada huo ulitolewa na Kaimu Balozi wa Poland nchini Tanzania Dk. Ewelina Lubieniecka na kupokelewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Amelchiory Kulwizila kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla katika hafla iliyofanyika katika Kijiji cha Ifupa Kata ya Ilungu Wilaya ya Mbeya mkoani hapa.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Balozi huyo alisema vifaa vilivyotolewa ni pamoja na vifaa kwa ajili ya Huduma ya Mama mjamzito kabla, Wakati na baada ya kujifungua vipatavyo 500 vyenye uwezo wa kuhudumia akina mama 5000 kwa wakati vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 69,750 sawa na yuro 27,900.

 

Alisema vifaa hivyo ni kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Ilungu ambacho kinajengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na wadau wengine hivyo msukumo wa kutoa vifaa hivyo ni pamoja na kuunga mkono na kuona juhudi za wananchi katika kuchangia maendeleo.

 

Aliongeza kuwa vifaa vingine vilivyotolewa ni pamoja na Viti 146, meza 34,stuli 75,Vitanda 123,Magodoro 89, Jiko la kupikia moja,Kabati za viatandani 31 na Pasi Moja kwa ajili ya Shule ya Sekondari ya Ilungu vyote vikiwa na thamani ya Shilingi Milioni 70.

 

Alisema vifaa hivyo vimetolewa na Kampuni ya Texpol ya nchini Polanda kwa ushirikiano na Shirika la Light for Afrika ambalo Mwenyekiti wake ni Julius Zellah  mkazi wa Polland na mzaliwa wa Ilungu mkoani Mbeya.

 

Akishukuru kwa ajili ya Msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Amelchiory Kulwizila alisema msaada huo utasaidia kuboresha huduma za afya katika Kata ya Ilungu na kuahidi kuleta Madaktari pindi Kituo hicho kitakapofunguliwa.

 

Aliongeza kuwa ili huduma zitakazotolewa ziwe na manufaa kwa jamii ni lazima kila Kaya ikakata Bima ya Afya kwa ajili ya matibabu jambo litakalosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

 

Awali Mbunge wa Jimbo la Mbeya vijijini, Oran Njeza alisema katika kuhakikisha Wananchi wanapata Bima kwa ajili ya Matibabu ataonesha mfano kwa kugharamia Kaya tatu tatu katika Vijiji 7 vya Kata hiyo ili wengine wahamasike kujikatia Bima wenyewe.

 

Naye Mganda wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Louis Chomboko  alisema uwepo wa Kituo cha Afya cha Kata ya Ilungu kitawapunguzia umbali wananchi wa kufuata matibabu katika Hospitali teule ya Wilaya iliyopo Ifisi ambako kuna umbali wa zaidi ya Kilomita 60.

 

Alisema mbali na umbali huo pia miundombinu ya barabara kutoka Kata hiyo hadi kufikia Hospitali ni mibovu jambo lililokuwa likihatarisha afya za wagonjwa wakati wakisafirishwa.

 

Mwisho.

 

 

UJUMBE KWA FACEBOOK