TTCL

Habari

Uvccm Mbeya Mjini Wamuunga mkono Rais Magufuli Kwa Hatua Alizochukua

on

   Mwenyekiti   wa Uvccm Wilaya Mbeya Mjini  Maranyingi  Matukuta akisoma tamko la kumpongeza Rais Magufuli mbele ya waandishi wa habari ambao hawapo pichani

TAMKO LA UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI(UVCCM) WILAYA YA MBEYA MJINI KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 27 MEI 2017, LA KUMUUNGA MKONO NA KUMPONGEZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DK JOHN JOSEPH POMBE MAGUFULI KWA HATUA ALIYOICHUKUA BAADA KUPOKEA RIPOTI YA KAMATI YA KUCHUNGUZA MCHANGA WA MADINI(MAKINIKA).

Ndugu waandishi wa habari, tumewaita na kuwaalika hapa kwa lengo la kuwaomba mtufikishie taarifa ya tamko letu kwa Watanzania wote kwa ujumla wao.

Awali ya yote tunawapongeza kwa kuendelea kutupa taarifa mbalimbali kama mhimili usio rasmi wa 4, hongereni sana ndugu zetu wanahabari.

Ndugu waandishi wa habari, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Wilaya ya Mbeya Mjini tunaunga mkono na kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Dk John Magufuli kwa hatua aliyoichukua dhidi ya viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini wanaoshughulika na madini pamoja na viongozi na watendaji wa Wakala wa vipimo wa madini Tanzania(TMAA).

Kwa mujibu wa Kamati iliyoteuliwa ilibeba dhamana ya kuchunguza na kupima makontena yaliyozuiliwa Bandarini, ilibaini udanganyifu na upotevu wa fedha kama sehemu ya ukwepaji wa kodi na kulikosesha Taifa mapato kwa ujanja wa watu wachache wakiwepo Watanzania waliokosa uzalendo kwa MAMA TANZANIA na zaidi waliangalia maslahi yao binafsi kuliko nchi kwa kushirikiana na Wawekezaji katika sekta hiyo ya madini.

Ndugu waandishi wa habari, Tumeona ripoti ya Kamati ilibaini uwepo wa madini mengine tofauti tofauti na dhahabu ambayo yanasafirishwa kwenye mchanga huo kinyume na utaratibu na hivyo kuwa na udanganyifu mkubwa ambao unatunyima Taifa mapato.

Nchi yetu imepata Neema ya Mungu kwa kuwa na Maliasili na Rasilimali mbalimbali lakini wapo baadhi ya Watanzania wenzetu waliopewa dhamana kulinda na kusimamia rasilimali hizo wameshindwa kufanya hivyo, watu hao wameamua kujilimbikizia mali kwa ufisadi na rushwa na kuiacha nchi yetu ikiwa maskini na omba omba wakati ina uwezo wa kujiendesha kwa bajeti ya mapato yake ya ndani.

Ndugu waandishi wa habari, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Mbeya Mjini tunaamini kuwa zile nyakati za kuishi kwa kulifisadi Taifa letu na kuligeuza kama SHAMBA LA BIBI kwa udanganyifu na maslahi binafsi sasa zimefikia mwisho kwenye awamu hii ya 5 chini ya uongozi wa Rais wetu Dk John Magufuli.
Tumeona viongozi na watendaji wengi wa serikali waliopewa dhamana na wengine walisomeshwa na Taifa letu wameshindwa kabisa kuwa wazalendo na badala yake wamekuwa wala rushwa na wabadilifu wa mali za umma na rasilimali za Taifa.

Ndugu waandishi wa habari, Mheshimiwa Rais Dk John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015, akitafuta kura na kuomba ridhaa ya uongozi wa nchi aliahidi na kuinadi ILANI YA UCHAGUZI YA CHAMA CHA MAPINDUZI kuwa chini ya serikali yake atahakikisha maliasili na rasilimali za nchi hii zinawanufaisha wananchi ambao wengi wao ni wanyonge na maskini.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Mbeya Mjini tunaona kabisa Rais Dk John Magufuli anayaishi na kuyasimamia maneno yake pia anafanya yale ambayo yapo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo ndio mkataba wa chama chetu na wananchi.

Ndugu waandishi wa habari, Tumeona tangu Rais Dk John Magufuli ameingia madarakani amefanya mambo mengi na makubwa yenye tija na manufaa kwa Taifa letu.

Tumeona mabadiliko kwenye sekta mbalimbali katika serikali na taasisi zake.
Tumeona nidhamu na heshima wa watumishi wa umma imerejea na watu wanachapa kazi bila ya mazoea.
Tumeona ongezeko katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ambayo ndio yanayofanya fedha ziende kwenye huduma za janii kama vile Afya, Elimu, Maji, Umeme, Miundombinu n.k

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mbeya Mjini tunawaomba Watanzania wote kuwa kwenye jambo lenye maslahi kwa Taifa kama hili suala la madini basi tuungane kwa pamoja, tushikamane na kupaza sauti zetu kupinga ufisadi na unyonyaji wa rasilimali za nchi yetu, kwa kufanya hivyo tunakuwa tumeungana na Rais wetu mpendwa Dk John Magufuli katika kutupeleka kwenye uchumi wa kati na uenda siku moja Tanzania tukawa nchi inayokopesha mataifa mengine fedha za maendeleo.
Tunawaomba watu wote ambao kwenye kila suala la maslahi na manufaa kwa nchi yetu wao wanapinga na kuleta siasa, vioja na kubeza waache mara maja, sisi hatuna Taifa jingine zaidi ya MAMA YETU TANZANIA.
Hivyo tuwe na mshikamano wa pamoja kuelekea katika Tanzabia Tuitakayo.

Ndugu waandishi wa habari, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi tumeona tusikae kimya zaidi ya kujitokeza mbele yenu kwa lengo la kuwafikishia tamko letu hili Watanzania pande zote Ulimwenguni kwa ajili ya kumuunga mkono na kumpongeza Mheshimiwa Rais Dk John Magufuli katika suala hili la mchanga wa madini pamoja na mambo mengi aliyoyafanya na anayoendekea kuyafanya na kuchukua hatua katika nchi yetu toka serikali ya awamu ya 5 imeingia madarakani.
Kwa mapendekezo ya Kamati ya hatua alizozichukua dhidi ya viongozi waliokuwa na dhamana katika sekta ta madini tunakubaliana nayo kabisa maana hakuna mkubwa zaidi ya Tanzania na cheo ni dhamana tu.

Tunamuomba Mheshimiwa Rais Dk Magufuli mara atakapopokea ripoti ya kamati ya pili ambayo ina wajumbe waliobobea katika masuala ya Uchumi na Sheria na ikibainika bado kuna ukiukwaji mkubwa zaidi na ujanja wa wawekezaji basi asisite kuangalia na kupitia upya mikataba ya madini kwa maslahi ya nchi yetu.

Ndugu waandishi wa habari, Mwisho, Tunawaomba Watanzania wote tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu Rais wetu mpendwa Dk John Magufuli aendelee kumjaalia afya njema na Baraka katika kuiongoza nchi yetu.
Tunawaomba Watanzania kuendelea kuiunga mkono na na kuwapa ushirikiano viongozi wa Serikali ya awamu ya 5 katika UTEKELEZAJI WA ILANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI 2015-2020.

Mungu Ibariki Tanzania.
Mungu Ibariki Afrika.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.

Imetolewa na;
Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Wilaya ya Mbeya Mjini.

UJUMBE KWA FACEBOOK