TTCL

Habari

WALIMU WAPIGWA MARUFUKU KUFANYA SIASA

on

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Mbarali mwishoni mwa Wiki. Mwenyekiti wa CWT Mbarali, Mwalimu Jailos Temba akisoma taarifa ya Chama hicho katika mkutano mkuu uliofanyika wilayani Mbarali mwishoni mwa wiki. Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune akiwaongoza viongozi wa Chama cha Walimu Wilaya ya Mbarali kuimba wimbo wa Mshikamano kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu wa Chama hicho. Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Walimu Wilaya ya Mbarali wakiwa kwenye mkutano mkuu wa Chama chao.

SERIKALI Wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya imepiga marufuku kwa Watumishi wa umma kujihusisha na Siasa hususani Walimu na kwamba wakibainika watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

 

Marufuku hivyo ilipigwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune alipokuwa akifungua Mkutano mkuu wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Mbarali kilichofanyika mwishoni mwa Wiki.

 

Alisema baadhi ya Walimu wamekuwa wakijihusisha na siasa katika maeneo ya kazi jambo ambalo linapelekea kuporomoka kwa ufaulu wa wanafunzi kutokana na kutumia muda mwingi kwenye harakati na sio kufundisha.

 

“Serikali ilikutuma mwalimu kufundisha na sio kujihusisha na harakati za kisiasa kwani kufanya hivyo kutapelekea kuibuka kwa makundi na ubaguzi na hatimaye kushindwa kufanya kazi uliyotumwa, hivyo suala la siasa waachie wanasiasa” alisema Dc.

 

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo Halmashauri ilishika nafasi ya mwisho ya ufaulu kwa matokeo ya darasa la Saba kwa Mkoa wa Mbeya  lakini baada ya kugundua makosa hivi sasa hali imeimarika.

 

Alisema katika matokeo ya mwaka huu ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 53 kwa mwaka jana na kufikia ufaulu wa asilimia 63 mwaka huu  jambo linaloashiria kuwepo kwa uwajibikaji kwa watendaji.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Mbarali, Mwalimu Jailos Temba alisema ili kuongezeka kwa viwango vya ufaulu Wakuu wa Idara, Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya watoke maofisini na kwenda kukutana na Walimu ili kujua changamoto zinazowakabili.

 

Alisema jambo lingine ni kuangalia namna ya kubadili ratiba ya wanafunzi kutoka shuleni kutoka vipindi viwili hadi kuwa kimoja kwa kuondoa muda wa kwenda kula mchana kutokana na mazingira wanayotoka wanafunzi.

 

Alisema asilimia kubwa wanafunzi wanatoka mbali na maeneo ya shule hivyo kupelekea wengi kushindwa kwenda kula huku wengine wakiwa hawawakuti walezi wao majumbani na kurudi shule bila kula na kupelekea kukosa usikivu mzuri.

 

Alisema ni vema utaratibu huo ukabadilishwa ili kuwawezesha wanafunzi wote kupumzika wakati walezi wapo majumbani ili waweze kupikiwa na kuongeza kuwa kundi linguine linaloathirika ni la watoto wa watumishi wa umma ambao muda wao wa kutoka ni saa tisa hivyo kukosa muda wa kuhudumia familia.

UJUMBE KWA FACEBOOK