TTCL

Habari

WANAOHUJUMU MIUNDOMBINU YA TTCL MBEYA WATIWA MBARONI

on

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwa wahalifu sita wa miundombinu ya Kampuni ya simu ya TTCL.

 

Meneja wa TTCL Mkoa wa Mbeya akielezea namna miundombinu ya Kampuni hiyo ya simu inavyohujumiwa na wahalifu kwa kuuzwa kama vyuma chakavu

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga akionesha nyaya zilizokamatwa katika operesheni maalum

Wahalifu ambao walikamatwa na nyaya za kampuni za TTCL wakiwa mbele ya vidhibiti walivyokutwa navyo

Mita za Maji za Mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira Jiji la Mbeya zikiwa zimekamatwa kutokana na Operesheni iliyofanyika hivi karibuni.

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu sita wakituhumiwa kuhujumu miundombinu ya Kampuni ya Simu za mkononi ya TTCL zikiwemo nyaya baada ya operesheni maalum.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga alisema Katika Operesheni hiyo jumla ya watuhumiwa walikamatwa wakiwa na nyaya za TTCL.

Aliwataja Watuhumiwa hao ni JACKSON NGALA [28] Mkazi wa Ilemi, MOSES SINYINZA [22] Mkazi wa Ilomba, LAURENT JONAS [30] Mkazi wa Forest Mpya, WILIAM JEREMIA [26] Mkazi wa Makondeko – Mwakibete, ANDREA JOSEPH [26] Mkazi wa Makondeko – Mwakibete na DICKSON FREDRICK [18] Mkazi wa Mama John – wote wa Jijini Mbeya.

Alisema siku za hivi karibuni Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilipata taarifa kuhusu uhalifu wa kuhujumu miundombinu ya Kampuni ya Mawasiliano Tanzania [TTCL] ambapo Katika uhalifu huo, wahalifu wamekuwa wanakata nyaya hizo kutoka kwenye nguzo na zingine kuzichimbua ardhini na kwenda kuuzwa kama vyuma chakavu.

Alisema Kutokana na taarifa hizo, Jeshi la Polisi liliunda kikosi kazi kwa kushirikiana na Maafisa wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania [TTCL] ili kubaini wahusika wanaoshiriki kufanya uhalifu huo.

Alisema Taarifa za kiintelijensia zilipatikana na kuanzia tarehe 31/12/2017 hadi tarehe 05/01/2018 Operesheni ilifanyika katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kuutia mbaroni mtandao wa wahalifu wanaojihusisha kuhujumu miundombinu ya TTCL kwa maana nyaya kwa kuzikata kwenye nguzo na zile zilizochimbuliwa ardhini.

Alisema pamoja na kuwatia mbaroni watuhumiwa, pia nyaya zilizohujumiwa za TTCL pamoja na Makampuni mengine kama TANESCO vilikamatwa katika maeneo ya watuhumiwa hao.

Aliongeza kuwa imebainika kuwa maeneo yaliyopata athari zaidi katika Mkoa wa Mbeya kutokana na kuharibiwa kwa miundombinu hiyo ni Eneo la Gombe – Itezi ambapo nyaya zenye urefu wa mita 150 zilikatwa,Eneo la Stendi Kuu ya Mabasi ambapo nyaya zenye urefu wa mita 50 zilikatwa,Eneo la Kiwanja Ngoma – Sokomatola ambapo nyaya zenye urefu wa mita 200 zilikatwa na Eneo la Ghana – Mbata nyaya zenye urefu wa mita 100 zilikatwa.

Kamanda Mpinga alisema katika Operesheni hiyo, mali mbalimbali ambazo ni nyaya za Kampuni ya Mawasiliano – TTCL zilikamatwa kama ifuatavyo,Nyaya zenye uzito wa kilogram 22.5 – Mali ya TTCL Mbeya,Mita za maji 08 [Reading Meters] Mali ya Idara ya Maji Mbeya na Nyaya zenye uzito wa kilogram 105 – Mali ya TANESCO Mbeya.

Hata hivyo alisema hadi sasa thamani halisi ya mali zote zilizopatikana bado haijafahamika, tunaendelea kuwasiliana na Idara husika kuweza kujua thamani halisi ya mali hizo.

Aliongeza kuwa Watuhumiwa wote mara baada ya kuhojiwa wamekiri kushiriki katika wizi na kuhujumu miundombinu ya Makampuni ya TTCL, TANESCO na Idara ya Maji.

UJUMBE KWA FACEBOOK