TTCL

Habari

WAZEE WA MILA MBEYA WAWAONYA WAKAZI WA ITUHA

on

Mkuu wa Machifu Mkoa wa Mbeya, Chifu Roketi Mwashinga akizungumza na wananchi wakazi wa Ituha Kata ya Ilomba jijini Mbeya ambapo amekemea Wakazi hao kuendekeza migogoro isiyokuwa ya lazima.

Mkuu wa Polisi Kata ya Ilomba, Dervard Mwalukuta akisisitiza jambo kwa wananchi wa Mtaa wa Ituha katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na viongozi wa Mila

Chifu Roketi Mwashinga akimpa maagizo Chifu wa Ituha kuhusu tabia za Wananchi kutumia jina la machifu vibaya kwa kujipimia maeneo na kuvamia sehemu ya CCM wakidai wameruhusiwa na Chifu wakati sio kweli.

Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Ituha, Leonard Mwazanya akifuatilia kwa makini Mkutano wa hadhara ulioitishwa na viongozi wa Mila Mkoa wa Mbeya

Baadhi ya Viongozi wa Mila Mkoa wa Mbeya wakiwa kwenye Mkutano wa hadhara Ituha Kata ya Ilomba jijini Mbeya

Eva Paul Mkazi wa Ituha jijini Mbeya akichangia jambo katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Machifu

Wakazi wa Ituha wakisikiliza kwa makini maagizo yanayotolewa na Chifu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya(hayupo pichani)

Baadhi ya Machifu wakiwa makini katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ituha jijini Mbeya

Baadhi ya vijana wakirekodi mazungumzo ya Chifu kupitia simu zao za mkononi

WAZEE wa Mila mkoani Mbeya wamekemea vikali tabia ya baadhi ya watu kuitukana Serikali na kudharau mamlaka zilizojuu yao ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uasi na vurugu kwenye jamii.

Wazee hao wakiongozwa na Chifu mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Roketi Mwashinga walisema Tanzania ni Nchi ya Amani hivyo hata fumbiwa macho mtu yeyote atakayetoa lugha chafu dhidi ya Serikali na viongozi.

Walitoa onyo hilo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mtaa wa Ituha Kata ya Ilomba jijini Mbeya kufuatia kuwepo kwa Mgogoro baina ya Wananchi na Chama cha Mapinduzi (CCM) wakigombea eneo la biashara.

Chifu Mwashinga akiwa ameongozana na wasaidizi wake zaidi ya 20 alisema Ituha kwa sasa si salama kutokana na kuwepo kwa ugomvi wa ajabu kwa baadhi ya watu kujichukulia sheria mkononi ili hali kesi ya msingi iko mahakamani.

Alisema Wananchi wa Ituha kwa hiari yao wenyewe walitoa eneo kwa CCM ambapo Chama kilifungua Tawi na kujenga vitega uchumi lakini hivi sasa baadhi ya watu wamejitokeza kudai maeneo hayo wakitumia mgongo wa machifu.

Aidha alikemea vikali baadhi ya watu kutumia vibaya jina la Chifu kwa kudai kuwa wameruhusiwa wakati hakuna Chifu mwenye eneo wala kilabu cha pombe na kwamba atakayeendelea ama kubainika atachukuliwa hatua kali.

“Mnaotumia vibaya majina ya machifu muache mara moja hakuna Chifu anayeshabikia migogoro kwani uwepo wao ni kukemea maovu kwa kusaidiana na Serikali, Hakuna Chifu mwenye kilabu isipokuwa tunachumba cha kunywea nyakati za jioni kwani hatuchanganyikani na watoto” alisema Chifu Mwashinga.

Nao machifu Paul Mwaigomole wa Ituha, George Lyoto wa Ilomba na Richard Mwanitengule wa Isyesye walisema vurugu zinazofanyika Ituha ni aibu kwa wazawa kwani eneo walitoa wenyewe kwa Chama na walishirikiana kujenga.

Kwa upande wake wakazi wa Ituha, Eva Paul na Mashaka Jonas walisema kinachowashangaza ni baadhi ya watu kuendeleza vurugu wakati kesi iko mahakamani ikisubiriwa hukumu kutolewa.

Walisema kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Machi 1, mwaka huu hivyo kuendekeza ugomvi kunapelekea kuzua hofu kwenye makazi yao na wengine kukimbia nyumba na kushindwa kushirikiana kwenye matukio ya kijamii.

Awali Katibu wa CCM Kata ya Ilomba, Yohana Mnyali alisema mgogoro wa kudai eneo hilo ulianzishwa na watu 9 mwaka 2006 wakidai eneo ni lao na kukimbilia mahakama ya ardhi Wilaya na kushindwa kesi na baadae kukata Rufaa lakini bado wakashindwa.

Alisema mwaka 2008 watu hao walikata Rufaa Mahakama kuu lakini nako hukumu ilitoka na kuipa ushindi CCM ambapo Mahakama ilitoa kibali kwa dalali kuwaondoa ili kukipisha Chama.

Aliongeza kuwa baada ya mabango ya kuwataka kuondoka kubandikwa kikaibuka kikundi kingine kinachoitwa Nsombe group club ambao wameenda mahakamani kukata rufaa ya kuondolewa tangu 2016.

Hata hivyo upande wa udalali, Highlands Auction Mart kupitia kwa Mkurugenzi wa Utekelezaji na Sheria, Fulco Mlelwa alisema pamoja na watu hao kukata rufaa bado jukumu la kuwaondoa lipo pale pale.

Alisema kisheria hawajaomba mahakama kusitisha zoezi la kuwaondoa hivyo wakati wowote wanapaswa kutii sheria kwa kupisha kwenye eneo hilo lenye ukubwa wa Hekta mbili kama Mahakama ilivyoamuru.

UJUMBE KWA FACEBOOK