TTCL

Habari

WAZIRI WA MAJI AFUNGA WIKI YA MAJI MBEYA

on

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akitoa hotuba ya kufunga maadhimisho ya wiki ya maji katika sherehe zilizofanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mbeya. Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akikipata maelezo ya Jengo la Utawala linalojengwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mbeya baada ya kuweka jiwe la Msingi. Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akisikiliza maelezo kutoka kwa mtaalam wa ufundi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mbeya. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mbeya, Mhandisi Simion Shauri akitoa maelezo kuhusu mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi kwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Kibao kikionesha Jiwe la Msingi likiwa limewekwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe.

 

KATIKA kuadhimisha wiki ya maji duniani, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya Mamlaka ya Maji safi na usafi waMazingira Jiji la Mbeya.

Sambamba na hilo Waziri pia alizungumza na wadau wa maji Mkoa wa Mbeya ambapo kwa pamoja walijadili changamoto na jitihada za kuhakikisha rasilimali za Maji zinatunzwa.

Aidha Waziri ameziagiza Mamlaka za Maji nchini kuhakikisha zinalipia huduma ya kuchukua maji kwenye mabonde kila mwezi ili kupata fedha za kusaidia utunzaji wa vyanzo vya maji.

Alisema ofisi za Mabonde ya maji zina majukumu makubwa ya kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa kwa ajili ya manufaa ya vizazi vilivyopo na vizazi vijavyo lakini yanakabiliwa na changamoto ya fedha hivyo njia pekee ni kupata kutoka kwenye mamlaka zinazochukua maji hayo.

Aidha alitoa wito kwa Mamlaka za Maji kuhakikisha zinadhibiti upotevu wa maji kwa kuwa unaingiza hasara kwa serikali kutokana na maji yanayopotea ni maji yaliyotibiwa na kusukumwa kwa umeme.

Alisema kiwango cha kimataifa cha upotevu wa maji hakitakiwi kuzidi asilimia 20 hivyo kila Mamlaka kuhakikisha hazizidi kiwango hicho ikiwa ni pamoja na kuondoa kabisa.

Awali akisoma taarifa kwa Waziri, Afisa Biashara wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mbeya, Venance Hawera kwa niaba ya Mkurugenzi alisema Mamlaka inamikakati ya kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kuwashirikisha wadau kwa kutumia ulinzi shirikishi.

Alisema mikakati mingine ni pamoja na kuongeza idadi ya wateja wa maji safi na maji taka mtandao wa maji uweze kuwafikia wananchi hadi majumbani kwao.

Aliongeza kuwa matarajio ya Mamlaka ni kuongeza chanzo cha maji kutoka Mto Kiwira uliopo Wilaya ya Rungwe ambacho kitazalisha Lita Milioni 65 kwa siku ujazo ambao utaongeza uzalishaji uliopo na kufikia Lita Milioni 115 kwa siku.

Alisema mradi huo wa maji kutoka Mto kiwira kilomita 37 kutoka Mbeya mjini utazalisha maji kwa njia ya mseleleko na kuongeza kiwango cha maji kitakachodumu hadi kufikia mwaka 2036 mradi ambao utagharimu shilingi Bilioni 42 hadi kukamilika.

 

 

UJUMBE KWA FACEBOOK