Habari

ZAHANATI NA SHULE KUPEWA FEDHA MOJA KWA MOJA KUTOKA SERIKALINI.

on

Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mbeya, Costantine Mushi akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya Uhasibu, uwekaji wa kumbukumbu kwenye vituo vya kutolea huduma katika sekta za Afya na Elimu. Mkufunzi na Mwenyekiti wa Watoaji wa Mafunzo, Dk. Oscar Gabone akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo kwa Wahasibu. Wahasibu wa sekta za Elimu na Afya wakiwa kwenye mafunzo Washiriki wakifuatilia mafunzo kwa makini Wahasibu wakiwa kwenye mafunzo ya Uhasibu na uwekaji kumbukumbu. Mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa mafunzo ya Uhasibu katika ukumbi wa Usungilo jijini Mbeya.

SERIKALI inatarajia kuanza kutoa fedha na kupeleka moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma zikwemo Sekta ya afya, Elimu, Serikali za vijiji na ofisi za Kata ili kuongeza uwajibikaji.

Hayo yamebainishwa wakati wa mafunzo kwa Wahasibu kuhusiana na uwekaji kumbukumbu za fedha na utoaji taarifa kwenye vituo vya kutolea huduma yanayofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Usungilo jijini Mbeya ukihusisha Halmashauri za Mikoa sita ya Nyanda za juu kusini.

Akimkaribisha mgeni rasmi Mwenyekiti mteule wa uendeshaji wa mafunzo hayo, Dk.Oscar Gabone ambaye pia ni Mkuu wa Taasisi ya Afya Iringa alisema kuanzia Julai mosi mwaka huu Serikali itaanza kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo vya afya, Shule na ofisi za Kata na Vijiji.

Alisema mfumo huo mpya utatoa motisha kwa vituo vya kutolea huduma za afya na kuongeza kipaumbele cha utoaji huduma bora kwa wananchi na kuongeza usawa na uwazi.

Aliongeza kuwa mfumo huo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa (FFARS) utasaidia utekelezaji wa utoaji wa rasilimali fedha moja kwa moja kwa ngazi za vituo vya kutolea huduma kwa kuimarisha uhitaji wa kuwepo kwa usimamizi wa fedha katika ngazi za vituo vya kutolea huduma.

Alisema mafunzo yameanza kwa wakufunzi 490 katika ngazi ya taifa na Halmashauri ambao watawawezesha watumishi katika vituo vya sekta ya Afya na elimu kupata ujuzi wa namna ya kutumia mfumo mpya wa FFARS.

Alisema wakufunzi hao wataweza kutoa elimu hiyo kwa watumiaji wa mwisho wa mfumo huo katika zaidi ya vituo vya afya 550, Zahanati 6800,Hospitali za Wilaya 135, Shule za Msingi na Sekondari 20,000 kwa Mikoa yote 26 ya Tanzania.

Awali akifungua mafunzo hayo,Mgeni rasmi  Katibu Tawala msaidizi Mkoa wa Mbeya, Costantine Mushi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alitoa wito kwa Wahasibu kuandaa majalada ya kunakili taarifa za fedha pindi zinmapotoka na kuingia ili kurahisisha utoaji wa taarifa wakati wa ukaguzi.

Alisema kumekuwa na mazoea kwa Wahasibu wengi kushindwa kutunza kumbukumbu za fedha jambo linalopelekea baadhi ya Halmashauri kupata hati chafu na zenye mashaka hivyo kupitia mfumo huo mpya utasadia kuboresha sekta ya fedha.

Mwisho.

 

UJUMBE KWA FACEBOOK